WAFUGAJI SAMAKI TANA RIVER KUFAIDI SOKO MBADALA LA SAMAKI
NA DENNIS MAITHYA
Wafugaji wa samaki kaunti ya Tana River sasa watapata fursa ya soko jipya la bidhaa zao baada ya kufanyiwa mafunzo ya njia mbadala za uuzaji wa nyama ya samaki kwa wateja wa ndani na nje ya kaunti.
Kwa mujibu wa Numias Kiti, mkufunzi wa maswala ya uvuvi kutoka shirika la Farm Africa , wakulima 112 wamepewa mafunzo ya kiufundi kuhusu ufugaji wa samaki huku wengine 105 wakipewa mafunzo ya kibiashara.
Numias kiti -mkufunzi wa ufugaji samaki shirika la Farm Africa. |
Mafunzo hayo amesema yamehusisha kuunganisha wafugaji wa samaki na soko ambapo sasa wataweza kuuza samaki kwa njia kama vile samosa,keki, kebab na baga, njia ambazo amesema zinaongeza thamani ya samaki na pia kuondolea wafugaji hasara ya samaki kuharibika haraka .
"kwasasa tumefunza wakulima 112 mafunzo ya kiufundi na wengine 105 kuhusu biashara. pia tumekuwa na maonyesho ya mauzo mbadala ya bidhaa za samaki kama vile kebab, samosa na vinginevyo ambavyo vitapanua soko na pia kuongeza thamani ya nyama ya samaki."
Vyakula mbalimbali kutoka nyama ya samaki |
Kulingana na Zablon Komora mfugaji wa samaki eneo la delta, uvuvi wa samaki mtoni umeathirika pakubwa kutokana na kubadilika kwa hali ya anga ,maji kupungua mtoni ambako kumechangia kupungua kwa samaki huku binadamu wakichangia kuchafua mto kutokana na shughuli zao za kila siku.
"changamoto saa hii ni kwamba hali ya anga imeanza kubadilika, hapa karibu na mto maji yamepungua na kusababishia samaki kuanza kupotea isitoshe wanadamu nao wameingilia mto kufanya shughuli ambazo zimeathiri kiwango cha maji na wengine hutupa uchafu mtoni unaoathiri samaki."
Zablon komora- mfugaji samaki Tana River |
Hata hivyo anasema kuwa mafunzo ya Farm Africa yamewasaidia huku sasa wakazi wanaojihusisha na biashara ya samaki wakizamia kukuza samaki kwa vidimbwi, hali anayosema imewawezesha kupata mkate wao wa kila siku pasi na kutegemea misimu mbalimbali wakati uvuvi hunoga.
Aidha amehoji kwamba ni rahisi kufanya biashara kwani mtu anaweza fanya ufugaji wa samaki nyumbani kwake.
"soko la samaki Tana River ni kubwa sana na mafunzo haya ya ufugaji wa samaki kwa vidimbwi ni ya manufaa kwa wakulima na jamii. maeneo mengi hapa Tana River yana mazingira mazuri ya kufuga samaki hivyo mtu anaweza akafuga samaki nyumbani kwake ama shambani na kujikimu kimaisha."
Anourd Meirgberg -mshauri wa kiufundi shirika la giz |
Anourd Meirgberg ambaye ni mshauri wa mambo ya kiufundi kutoka shirika la kijerumani GIZ, ufugaji wa samaki kwa vidimbwi utawezesha wafugaji kufanya biashara yao pasi na kuzingatia misimu pekee.
Hilo anasema litaongeza kipato kwa wafanyibiashara ambao wataweza kufanya mahesabu yao na kujua kiwango cha fedha wanachotarajia kutokana na idadi au aina ya samaki wanaofuga.
Comments
Post a Comment