SHIRIKA LA MSALABA MWEKUNDU KUCHINJA NG'OMBE 730 TANA RIVER AWAMU YA PILI YA MRADI WA SERIKALI

 NA DENNIS MAITHYA

Shirika la msalaba mwekundu kupitia serikali kuu limeanza awamu ya pili ya mpango wa kununua na kuchinja mifugo iliyodhoofika kaunti ya Tana River.

Mratibu wa shirika hilo hapa Tana River Gerald Bombe amesema kuwa awamu hiyo ya pili ambayo ilianza tarehe mbili septemba inalenga kuchinja ng’ombe 730 kote kaunti hii.

Katika awamu ya kwanza ya mpango huo iliyotamatika mwishoni mwa Julai, Bombe amebaini kuwa walichinja ng’ombe 525 kati ya 1,255 wanaolengwa kaunti nzima.

“Katika awamu ya kwanza tulinunua na kuchinja ng’ombe 525. Delta ngo’mbe 84 na mbuzi 419, Tana Kaskazini ng’ombe 138 na mbuzi 131, Galole ng’ombe 138 na mbuzi 89.”

Gerald Bombe- mratibu Redcross Tana River

Kulingana na Bombe, Ng’ombe mmoja ananunuliwa kwa shilingi 15,000 na mbuzi au kondoo kwa shilingi 3,000.

“Bei iliyowekwa kununua mifugo ni sawa katika kaunti zote zinazoshiriki mpango huu. Tunalenga wafugaji ambao wanahisi kuwa mifugo wao wamedhoofika kiasi kwamba hawaezi kustahimili hadi mvua itakaponyesha.”


Hayo yanajiri huku baadhi wafugaji eneo la Kalkacha awamu ya pili ilikozinduliwa wakitaka serikali angalau kuongeza kiwango cha pesa kwa mifugo waliodhoofika hadi angalau shilingi elfu ishirini na tano.

Isaack Dara mfugaji eneo hilo amesema kuwa kati ya mifugo wake 150, amesalia na 25 pekee ambao amehamishia eneo la Tana Delta ambalo angalau lishe kiasi inapatikana.

“Nina miaka 54, ukame ambao umetupata mwaka huu ni wa kushangaza. Mimi binafsi nilikuwa na ng’ombe 150, nimesalia na 25 ambao nimehamishia eneo la Witu kwasababu tuliko ni kukavu.”

Maafisa wakagua usalama wa nyama

Omar Godana mfugaji  mwengine amekiri kuwa ukame umewasukuma pabaya na hata nyakati zingine kusababisha utata baina ya wakulima wa mimea na wale wanaofuga.

“wanyama wameisha, maji hakuna tunategemea mto na wakati mwingine inazua utata baina ya jamii.kwasasa tunategemea visima ambavyo unaweza chimba asubuhi maji yakatoka saa tisa jioni mifugo wanywe.”

Ameongeza kuwa hali hiyo ya ukame imepelekea bei ya mifugo kuwa duni. Kulingana naye bei ya fahali siku za kawaida hufika hadi elfu 70 lakini kwasasa hata kwa shilingi elfu 25 na wale wa chini kabisa shilingi elfu kumi, bei ya zamani ya mbuzi.



Esha Guyole ametaka serikali kuongeza mbinu za msaada kunusuru hali kwani kwasasa kina mama na watoto wanakumbwa na njaa kupindukia.Badala ya lishe ya nyama jamii inayopata katika mpango huo, amependekeza njia zingine za lishe.

“Jameni, ng’ombe mwenyewe anayechinjwa hana nguvu, je sisi tunaokula hiyo nyama si tutazidi kukonda? Badala yake afadhali tusaidiwe na njia nyingine ya lishe.”



Kwa mujibu wa Bombe, mpango huo unaratibiwa kutamatika baada ya wiki mbili. Kando na hayo amebaini kuwa shirika la msalaba mwekundu linaendelea na mipango mingine ya kukabili makali ya ukame.

Miongoni mwa mipango hiyo ugavi wa chakula cha msaada kwa familia 5,000 kwa ushirikiano na shirika la mpango wa chakula duniani (WFP), Mpango wa kuboresha mazingira kupitia upanzi wa miti Climate Smart na mingineyo.

Comments

Popular posts from this blog

NG'OMBE 1,036 TANA RIVER KUCHINJWA KATIKA MPANGO WA SERIKALI KUKABILI MAKALI YA KIANGAZI NCHINI

TANA RIVER : BARAZA LA WANAHABARI NCHINI (MCK) LAHIMIZA USHIRIKIANO BAINA YA WANAHABARI NA UMMA

TANA RIVER : WANASIASA WAONYWA DHIDI YA SEMI ZA CHUKI NA KAMPENI ZA USIKU