TANARIVER KAUNTI YA 4 KENYA KUZINDUA MWONGOZO UTAKAOSAIDIA KUKOMESHA UKEKETAJI

(Kutoka kushoto) Abas Kunyo waziri jinsia Tana River,Thomas Sankei kamishna wa Tana River,Nyerere Kutwa Anti fgm Board na Khalif Hassan mkurugenzi wa elimu Tana River


NA DENNIS MAITHYA

Kaunti ya Tana River imekuwa kaunti ya hivi karibuni baada ya kaunti za Kisii, Migori na Garissa kuzindua mwongozo wa kukabiliana na ukeketaji. 

Haya yamejiri baada ya kaunti hii Alhamisi tarehe 26 Mei 2022 kuzindua mwongozo wa kukabiliana na ukeketaji hadi mwaka 2025.

Kulingana na ripoti moja ya shirika la UNICEF inakisiwa kwamba karibu wasichana na wanawake milioni 200 katika mataifa zaidi ya 30 duniani wamekeketwa. Ripoti hiyo aidha inaonyesha hapa kenya karibu wasichana na wanawake milioni tisa na laki tatu wamekeketwa.

Kwa mujibu wa ripoti nyingine ya mwaka 2014 ya afya ya watu nchini (KDHS 2014) kiwango cha ukeketaji hapa nchini kwa wasichana na wanawake kati ya miaka 15 hadi 49 ilikuwa asilimia 21 mwaka 2014.

Hapa Tana River kiwango cha ukeketaji ni asilimia 58 kulingana na ripoti hiyo huku jamii tano Orma,Wardei,Watta,Munyoyaya na Wailwana zikitajwa kufanya ukeketaji kwa kiwango kikubwa.

wadau wapokezwa nakala za mwongozo

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la WomanKind Kenya mwaka 2021, inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya wasichana na wanawake kutoka jamii zinazoshiriki ukeketaji Tana River wamepitia tendo hilo, huku ikibainika zaidi kuwa kuna ufahamu wa chini kuhusu athari za ukeketaji na haki za wanawake na wasichana.

Sababu zilizotajwa kuchangia ukeketaji ni ikiwemo utamaduni,uchumi,dini na imani,dhana potofu na ubaguzi ambazo zimehusishwa pakubwa kuchochea tendo hilo.

Hata hivyo uzinduzi wa mwongozo huo umepigiwa upatu kukomesha ukeketaji kwa kuhusisha jamii na washikadau kufuata mkondo sambamba katika makabiliano yake.

Kamishna wa kaunti hii Thomas Sankei amekariri kuwa ukeketaji ni tendo lililopitwa na wakati na halistahili kushuhudiwa katika kizazi cha leo.

"Aliyeanzisha ukeketaji alikuwa na nia yake lakini je sisi tunafanya kwa nia gani? Hatuwezi fanya kitu kwasababu kilifanywa tu.kikweli FGM haina dhamana kwetu watu wa kisasa."Amesema Sankei.

Thomas Sankei -kamishna Tana River

Akipongeza Tana River kwa hatua za kukabiliana na ukeketaji, meneja wa mipango katika bodi ya kitaifa ya kukabili ukeketaji Nyerere Kutwa amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau kaunti hii kuafikia ruwaza ya rais Uhuru Kenyatta kukomesha ukeketaji mwaka  wa 2022.

"Napongeza Tana River kuwa  ya nne kati ya kaunti  22 kuzindua mwongozo huu. Tutaendelea kushirikiana nanyi ili tuafikie ruwaza ya rais na pia kulinda haki za watoto wetu."Amesema Kutwa.

Aidha mwa mujibu wa waziri katika idara  jinsia kaunti hii Abass Kunyo ipo haja ya kukomesha ukeketaji kwani umelemaza elimu na maendeleo ya mtoto wa kike kutokana yanayojiri baada ya kuketwa.

"Kulingana na tamaduni, msichana anapokeketwa amevuka kiwango kingine cha maisha na anadhamiriwa kuwa tayari kuanza familia, hivyo mambo ya elimu yanakatizwa." Amesema Kunyo.

Kwa kauli ya pamoja baada ya kurasmisha mwongozo huo, wadau wote husika wameahidi kushirikiana kukomesha ukeketaji.

wadau kwenye uzinduzi wa mwongozo

Mwongozo huo umebuniwa kwa mchango wa serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti ya Tana River kupitia Shirika la Unicef,bodi ya kitaifa kupambana na ukeketaji,Womankind Kenya na Plan International.



Comments

Popular posts from this blog

NG'OMBE 1,036 TANA RIVER KUCHINJWA KATIKA MPANGO WA SERIKALI KUKABILI MAKALI YA KIANGAZI NCHINI

TANA RIVER : BARAZA LA WANAHABARI NCHINI (MCK) LAHIMIZA USHIRIKIANO BAINA YA WANAHABARI NA UMMA

TANA RIVER : WANASIASA WAONYWA DHIDI YA SEMI ZA CHUKI NA KAMPENI ZA USIKU