TANA RIVER : BARAZA LA WANAHABARI NCHINI (MCK) LAHIMIZA USHIRIKIANO BAINA YA WANAHABARI NA UMMA
NA DENNIS MAITHYA.
Mratibu wa baraza la kitaifa la wanahabari nchini (MCK) eneo la pwani Bi. Maureen Mudi ametoa wito kwa wanahabari kuzingatia kanuni za uanahabari msimu huu wa uchaguzi ili kuhakikisha usawa wa utoaji habari .
Akizungumza katika kongamano lililokutanisha mck, wanahabari na washikadau wengine mjini Hola kaunti ya Tana River, Mudi ameelezea umuhimu wa ushirikiano baina ya asasi mbalimbali za jamii na wahabari , pamoja na umma kufahamu utendakazi wa wanahabari.
"Kongamano hili linakutanisha wananchi wa mashinani na wanahabari kuwaeleza utendakazi wa wanahabari na majukumu ya vyombo vya habari ikiwemo utoaji wa habari kwa njia zinazostahili ."
Mratibu huyo ameongeza kuwa baraza la kitaifa la wanahabari limeandaa misururu ya mafunzo kwa wanahabari uchaguzi mkuu unapowadia ili kuhakikisha wanaripoti matukio yanayohusiana na uchaguzi kwa njia ya usawa.
"kama mck tumekuwa tukifanya mafunzo kwa wanahabari tunapoelekea uchaguzini.Himizo langu ni kwamba watoe taarifa zisizoegemea upande mmoja, na pia wana wajibu kuhakikisha kenya haitarudi kwa wakati wa uchaguzi wa utata na vurugu."
Ili kufanikisha utendakazi mwema wa wanahabari katika uchaguzi, Bi. Mudi amebaini kuwa MCK inapania kutenga sehemu maalum karibu na vituo vya kuhesabia kura kwa wanahabari kuchapisha na kutoa taarifa zao kwa wakati ufaao . Hilo amesema litapunguzia wanahabari changamoto za kutafuta sehemu za kutuma taarifa kwa vituo vyao.
"wiki iliyopita tumekuwa tukitafuta maeneo katika kila ukanda tuliyopo tuweke vituo vya wanahabari kufanya kazi zao hususan maeneo karibu na vituo vya kuhesabia kura ili wafanye kazi zao bila kutatizwa ama kuhangaika kutafuta sehemu maalum kutuma taarifa."
Kando na vituo hivyo vya kufanyia kazi, ameongeza kuwa wanahabari nchini wataweza kuthibitisha uhalisia wa habari zinazochapishwa katika mitandao ya kijamii ili kujiepusha na uwezekano wowote wa kusambaza taarifa zisizo kweli kupitia mtandao maalum uliobuniwa kuwawezesha kubaini ukweli wa taarifa hizo.
Hayo yanajiri huku washikadau kaunti ya Tana River wakipongeza vituo vya habari kaunti hiyo kwa ushirikiano mwema katika kuangazia maswala ya kijamii.
Kulingana na Ruth Kaseme , mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake gatuzi dogo la Tana River, kongamano hilo limekuwa faafu wakati huu kwani limewawezesha kupata maelezo kuhusu utendakazi wa wanahabari.
"kongamano hili limekuwa la muhimu sana kwasababu tushajua jinsi wanahabari wanafanya kazi na kama kuna shida yoyote tumewapata jinsi ya kuwasiliana nao.kwasasa uhusiano wetu nao upo sawa."
Ruth Kaseme-mkazi Tana River |
Yasmin Hassan, naibu mwenyekiti wa baraza la vijana kaunti ya Tana River amesema warsha hiyo imewasaidia kufahamu jinsi ya kushirikisha wanahabari kuangazia maswala yao.
Comments
Post a Comment