TANA RIVER : WANASIASA WAONYWA DHIDI YA SEMI ZA CHUKI NA KAMPENI ZA USIKU
Akiongoza msafara wa matembezi ya kuhamasisha amani katika mji wa Hola Jumatano wiki hii, Lenkarie amesema kuwa serikali ipo makini sana kuhakikisha hakuna mwanasiasa atakaye vuruga amani ya jamii kwa kutoa kauli za chuki na uchochezi.
"wale wanaongea semi za chuki na kuchochea tutawachukulia hatua. watu wetu wako kwa nyanjani wanasikiliza vile mnaendelea."
Naibu kamishna Tana River Joseph Lenkarie |
Kadhalika ametoa onyo kwa wanasiasa watakao kiuka sheria zilizowekwa za kufanya kampeni huku akiwataka kuzingatia muda uliotengwa kufanya shughuli hiyo ya utafutaji kura.
"Hata wale ambao wanafanya mambo yao usiku. Kampeni ni kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. yale masaa hayaruhusiwi tuwache."
Lenkarie amehakikisha kuwa serikali itashirikiana na kamati za amani kaunti hiyo huku akisihi kamati hizo kuwa tayari wakati wowote wakihitajika .
Msafara huo wa amani vile vile ulivutia baadhi ya wanasiasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kaunti ya Tana River, wote wakihimiza wakazi na wanasiasa wenzao kudumisha amani wakati uliosalia wa kampeni, wakati na hata baada ya uchaguzi.
"Lengo letu viongozi ni kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi wa amani. mwananchi apige kura kwa amani na arudi kusubiri matokeo kwa amani." Alisema Ali Dhadho mgombea wa uwakilishi wadi chewani.
Mgombea mwingine wa uwakilishi wadi ya Chewani Richard Ogwoka ametoa wito kwa jamii kuwapa nafasi wagombea viti mbalimbali kuuza sera zao ili wapate kiongozi aliye na mipango bora zaidi kwa wakazi.
"Kama kiongozi yeyote anakuja kwenu kuuza sera nyinyi kama wananchi mkae chini msikilize amalize aondoke, mwingine akija vivyo hivyo . siku ya kura mtaamua wenyewe ni nani mwenye sera za kutatua matatizo yaliyomo ."
Aidha amepongeza wakazi wa Tana River kwa kudumisha amani akisema kuwa kwasasa anahisi kuna ukomavu wa kisiasa kwani hakuna sehemu yoyote Tana River ambayo imeripotiwa kushuhudia fujo wakati wa kampeni.
Ibrahim Wayu anayegombea kiti cha uwakilishi wadi Mikinduni aidha amesisitiza uwepo wa amani ambayo anasema ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya kiuchumi na endapo inakosekana shughuli nyingi za kibiashara zitaathirika.
Comments
Post a Comment