POLISI TANA RIVER WAOMBEWA UCHAGUZI MKUU UKIWADIA
NA DENNIS MAITHYA
Maafisa wa Polisi kaunti ya Tana River wamefanyiwa maombi maalum wanapojiandaa kuhudumia taifa katika uchaguzi mkuu wa Agosti tisa mwaka huu.
Kamanda wa polisi gatuzi dogo la Tana Kaskazini Ali Ndiema amesema ibada hiyo ya maombi imewafaa sana maafisa wa polisi wanapojiandaa kwa uchaguzi mkuu nchini.
Ndiema amesema kuwa nyakati za ibada angalau maafisa hunawiri ki imani na hata kisaikolojia kwani wanapotangamana na wenzao wanabadilishana hisia na mawazo.
" Ibada hizi huwaleta maafisa wa polisi pamoja kupata baraka,kujengeka kiroho na hata kisaikolojia, hasa wakati huu tunapoelekea uchaguzini tumejazwa nguvu na bila shaka tunarajia uchaguzi mwema."
Ali Ndiema(katikati) kamanda wa polisi gatuzi dogo la Tana North. |
Aidha amebaini kuwa maafisa wamepewa mwongozo tosha wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao katika uchaguzi kama tume ya uchaguzi IEBC inavyoelekeza.
"Tumezungumza na maafisa wetu na wanafahamu wanavyotakikana kufanya kazi kuhakikisha uchaguzi salama.lengo letu kuu ni kutoa ulinzi na kuhakikisha uchaguzi unakamilika vizuri."
maafisa wa polisi katika ibada |
Kwa mujibu wa mchungaji Isaac Magabe wa kanisa la Christian International aliyeongoza ibada hiyo ya maombi, maafisa wa polisi wanahitaji ulinzi wa Maulana wanapokuwa kazini msimu huu wa uchaguzi.
Mchungaji Isaac Magabe wa kanisa la Christian International Hola |
Kwa upande wake kasisi wa huduma za polisi kaunti ya Tana River Amon Mwadeghu ibada ya maombi kuombea maafisa wa polisi na amani katika uchaguzi imekuwa ya baraka na sasa maafisa watafanya kazi kwa weledi na ujasiri.
"Bila ulinzi wa Mungu hatuwezi,naamini kupitia maombi haya maafisa wetu sasa watafanya kazi popote watakapotumwa kwa ujasiri."
Kasisi Amon Mwadeghu wa huduma za polisi Tana River |
Ibada hiyo ya maombi iliyofanyika jumamosi tarehe 25 Juni 2022 imevutia maafisa wa polisi kutoka magatuzi madogo yote ya Tana River.
Comments
Post a Comment