TANA RIVER: WAGOMBEA TANO KATI YA 12 WANAOWANIA KITI CHA SENETI WAIDHINISHWA RASMI NA IEBC KUFIKIA SIKU YA PILI
NA DENNIS MAITHYA
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kwa siku ya pili imeendelea kukagua stakabadhi za wanasiasa wanaowania viti mbalimbali vya kisiasa ili kuwaidhinisha rasmi kama wagombea wa viti hivyo.
Kufikia leo jioni tarehe 30 Mei, meneja wa uchaguzi kaunti ya Tana River Yonah Ogalo amedhibitisha tume hiyo kuidhinisha rasmi wagombea tano wa kiti cha seneti, idadi hiyo ikiwa ni asilimia 41.6 ya jumla ya wawaniaji kumi na wawili wanaotarajiwa kuwasilisha stakabadhi zao.
Yonah Ogalo , meneja wa uchaguzi Tana River akiongea na wanahabari kwenye kituo cha kuidhinisha maseneta. |
Miongoni mwa wagombea tano wa useneti walioidhinishwa rasmi kufikia sasa ni aliyekuwa seneta wa kwanza wa Tana River Ali Bule anayewania kupitia chama cha Federal Party of Kenya (FPK).
Ali Bule aliyekuwa seneta wa Tana River |
Danson Mungata , aliyekuwa mbunge wa Garsen ambaye sasa anawania useneta kupitia chama cha UDA kilicho kwenye muungano wa Kenya kwanza chini ya uongozi wa naibu Rais William Ruto.
Danson Mungatana (katikati) baada ya kuidhinishwa |
Kigogo mwengine aliyeidhinishwa ni aliyekuwa mbunge wa Galole Hassan Dukicha almaarufu "Gorfo Kayyo" ambaye sasa anawania kiti hicho kupitia chama cha Jubilee kilichopo kwenye Muungano wa Azimio One Kenya .
Hassan Dukicha (kushoto) akipokezwa cheti cha kuidhinishwa |
Chama kipya cha Pamoja African Alliance kinachoongozwa na gavana wa Kilifi Amason Kingi aidha kitawakilishwa na Bakari Garisse.
Bakari Garisse (katikati) baada ya kupokea cheti kutoka IEBC |
Sadam Salat mchanga zaidi kwenye orodha ya wagombea kiti hicho walioidhinishwa kufikia sasa atapeperusha bendera ya chama cha ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi.
Sadam Salat (kushoto) akipewa cheti na Yonah Ogalo meneja wa uchaguzi Tana River |
Wagombea baada ya kuidhinishwa wametoa wito kwa washindani wote kufanya siasa za amani zinazozingatia sera.
wakati uo huo Mungatana ametuma risala za rambi rambu kwa ndugu na jamaa za mbunge wa Rabai William Kamoti wa ODM aliyefariki kwenye ajali ya barabarani saa chache baada ya kuidhinishwa na IEBC kutetea kiti chake.
"Natoa rambirambi zangu kwa familia ya marehemu william Kamoti ambaye alikuwa wakili mwenzangu na wakazi wa Rabai kwa jumla na kwa chama chake pia ODM kilikuwa kimeshakamilisha mipango yake."Mungatana.
Hapo kesho tarehe 31 wawaniaji 7 kati ya walioonyesha azma yao wanatarajiwa kufika ikiwa ni siku ya tatu kama ilivyoratibiwa na IEBC.
Baadhi ya wanaotarajiwa ni Seneta wa sasa Juma Wario,aliyekuwa naibu gavana Jire Siyat na Maur Bwanamaka miongoni mwa wengine.
Comments
Post a Comment