SIKU YA USAFI WA HEDHI DUNIANI: WADAU TANA RIVER WATAKA HAMASA KUFANYWA ZAIDI MASHINANI.


watoto wa kike wafurahia kupokea sodo na sabuni katika maadhimisho ya siku ya usafi wa hedhi.

NA DENNIS MAITHYA.

Huku ulimwengu mzima ukiadhimisha siku ya usafi wa hedhi , Kaunti ya Tana River imeungana na maeneo mengine kuadhimisha siku hiyo katika shule ya msingi ya Kalkacha, kata ya Kalkacha gatuzi dogo la Tana River.

Hafla hiyo imevutia wasichana kutoka eneo hilo na viunga vyake, wengi wakiwa na matarajio ya kuelimishwa kuhusu usafi wa hedhi na angalau kupata sodo kama ishara ya kuashiria usafi wa hedhi.

Chifu wa eneo hilo Osman Dara amebaini kuwa changamoto za siku za hedhi huwafanya wasichana wengi eneo hilo kutohudhuria shule, sababu zikiwemo kukosa sodo au hedhi kuchukuliwa kwa usiri.

"Watoto wakiwa katika hali hizo wengi hawaendi shule , jambo hilo pia huchukuliwa kwa usiri mkubwa halizungumziwi na wazazi." Amesema Osman.

 

Chifu kalkacha Osman Dara

 Kulingana na afisa wa afya ya uzazi katika hospitali ya rufaa ya Hola daktari Hawa Abdulghafoor , siku hii ina umuhimu sana Tana River kwani matumizi ya sodo bado yamekuwa nadra kwa watoto wa kike kwasababu wamekuwa awali wakitumia mitindo ya kale isiyo salama siku za hedhi.

"Matumizi ya sodo awali yamekuwa nadra kwa msichana wa Tana River kwani walitumia mbinu za kale kama kutumia vitambara au kuchimba vishimo ili kujisaidia jambo lililohuzunisha sana."Amesema dkt. Hawa.

Hata hivyo amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwahusisha vijana  wa kiume na wazazi ili kuondoa dhana ya hedhi kuwa jambo la kike pekee bali ni hali ya kawaida ndiposa msichana ajihisi huru anapoona mwezi.

Dkt.Hawa Abdulghafoor afisa wa afya ya uzazi akipokeza wasichana sodo.

Milka Hadida, mmoja wa afisa kujitolea wa shirika la msalaba mwekundu kadhalika ametaja uhaba wa visodo kuchangia wasichana kutumia njia mbadala kujisaidia nyakati za hedhi. Ameongeza kuwa isingalikuwa ni mashirika yasiyo ya kiserikali hali ingelikuwa ngumu zaidi.

"wasichana wengine mpaka saa hizi wanatumia magodoro,madera au vitambaa kuukuu kama sodo.imekuwa ngumu sana kwasababu wanaosaidia aghalabu ni mashirika yasiyo ya kiserikali."

 

Milka Hadida (kulia) akigawa sodo kwa wasichana waliojitokeza sherehe ya usafi wa hedhi Kalkacha.

Fauka ya hayo, Ralia Buyothu ,mtetezi wa haki za kijinsia amenyoosha kidole cha lawama kwa kile amedai ni maandalizi duni ya sherehe hiyo kubwa ambayo ilistahili kuleta pamoja wadau wengi kuchangia visodo na vifaa vingine vya usafi.

"Idara husika zingetangaza hata angalau wiki moja ili ujumbe ufike kwa walengwa wengi ambao kwasasa wanapitia changamoto za kiuchumi kupata sodo.wangejifunza mengi kwa siku hii." 

Buyothu ameongeza kuwa wasichana kutoka jamii za wafugaji Tana River ndio wenye changamoto zaidi na kwamba elimu hiyo inafaa kuwafikia huko mashinani,akipendekeza sherehe hiyo kupelekwa vijijini zaidi.

 "Mpaka saa hii kunao wasiotumia visodo . Wako huko mashinani zaidi wanatumia desturi za zamani.wakati mwingine hii sherehe ipelekwe huko,sehemu kama kalalani,Asa kone, kone kaliti na kwingine  hao ndio wanahitaji hii elimu zaidi angalau hawa wa mjini wana ufahamu zaidi kwasasa."

Mtetezi huyo amedokeza kuwa kutokana na ukosefu wa elimu ya usafi wa hedhi na kutokuwa na uwezo wa kupata vifaa hivyo hufanya wasichana kutumia mbinu za kitambo ambazo zinawahatarisha kupata magonjwa ya sehemu za kizazi.

Kupitia juhudi za wadau waliochangia, angalau wasichana 30 kati ya zaidi ya 200 waliojitokeza walipokea sodo pakiti moja kila mmoja na sabuni, wadau wengine na mashirika wakiombwa kuweka mkono katika maswala ya elimu ya usafi wa hedhi.




Comments

Popular posts from this blog

NG'OMBE 1,036 TANA RIVER KUCHINJWA KATIKA MPANGO WA SERIKALI KUKABILI MAKALI YA KIANGAZI NCHINI

TANA RIVER : BARAZA LA WANAHABARI NCHINI (MCK) LAHIMIZA USHIRIKIANO BAINA YA WANAHABARI NA UMMA

TANA RIVER : WANASIASA WAONYWA DHIDI YA SEMI ZA CHUKI NA KAMPENI ZA USIKU