MRADI WA SHARED FUTURES KUFAIDI VIJANA ELFU MOJA TANARIVER.
Angalau vijana elfu moja na watu wazima kaunti ya Tanariver wanatazamiwa kufaidi mradi wa miaka miwili na nusu wa majaribio unaolenga kuhusisha vijana katika Nyanja mbambali kwa malengo ya kukabili itikadi kali katika jamii.
Mradi huo SHARED FUTURES ambao upo katika awamu ya pili utatekelezwa na mashirika tano yakiwemo Africa Youth Trust, Jamii action Centre,Samba sports Agenda, ADS pwani na CORDAID.
Kulingana na Mohammed Mwachausa wa shirika la Samba sports Agenda nia na madhumuni ya mradi huo utakaojumuisha mipango mbalimbali ya kuhusisha vijana kaunti hii ikiwemo maswala ya kilimo biashara, michezo na Sanaa pamoja na utangamano wa kidini ni kuhakikisha vijana wanahusishwa ili kuwaweka katika mazingira faafu yatakayowaondolea mafikira ya kujihusisha na makundi haramu na itikadi kali.
"Vijana wanapokuwa wanawachwa pekee yao na labda wana ukiwa au upweke wanajihisi kuwa wamesukumwa na jamii na serikali wajifanyie mambo kivyao mara nyingi wanakuwa na hasira na serikali, wazazi na vitengo vya usalama hapo wanapata hisia za kulipiza kisasi." Alisema Mwachausa.
Pamwe na hayo, Elizabeth Righa wa shirika la ADS pwani ameongeza kuwa wanapania kuhusisha watoto wa kike katika mafunzo muhimu kama vile ya uzazi , na kuwaelimisha dhidi ya mimba za utotoni, ndoa za mapema na vilevile dhulma za kijinsia na unyanyasaji.
"Tumegundua tulipokuwa tunafanya shared futures awamu ya kwanza tulipata changamoto kama vile mimba na ndoa za utotoni kwa wanarika, dhulma za kijinsia kwa familia na wanakosa pa kukimbilia. Nguzo ya tatu ya mwongozo wa kukabili itikadi kali itaangazia kushughulikia hayo." Alisema Righa.
Hayo yamejiri mjini Hola katika kikao cha washikadau wanaokabili itikadi kali. Ikumbukwe kaunti ya TanaRiver ilizindua mwongozo wa kuelekeza mikakati dhidi ya itikadi kali mwaka 2019. Mwongozo huo umekuwa na nguzo kumi na moja ambazo asasi mbalimbali zimekuwa zikitekeleza yaliyomo kwenye nguzo hizo.
Comments
Post a Comment