MPUNGA HATARINI KUKAUKA BURA KWA KUKOSA MAJI
Wakulima wa mpunga katika mashamba ya Bura wamelalamikia kukauka kwa baadhi ya mashamba kutokana na ukosefu wa maji ya kutosha .
Wakiongea na wanahabari mjini Bura , wakulima hao wanasema kuwa awali walipokuwa wakipanda mahindi hawakuwa na changamoto nyingi za maji ila tangia waanze kilimo cha mpunga kinachonoga kwa sasa wamekumbwa na upungufu wa maji mara kwa mara. "Tulipokuwa katika mradi wa kenya seed hatukushuhudia changamoto za maji lakini tangu tuanze mpunga tatizo la maji limekithiri kwasababu mpunga wahitaji maji mengi kunawiri." Alisema Lucy Wangari mmoja wa wakulima.
Peter Muchai , mkulima mwingine amebaini kuwa baadhi ya wakulima katika mashamba hayo wanakadiria hasara kutokana na kukauka kwa mazao yao , tatizo kuu likiwa ukosefu wa maji ya kutosha mashambani. "Saa hii ukitembea kwa haya mashamba, mengi yameungua kwasababu ya ukosefu wa maji, tungepata maji ya kutosheleza kila mkulima hatungeomba msaada, shida haya maji tunapimiwa kama dawa." Amesema Muchai.
Kulingana naye tatizo kubwa lipo katika kusukuma maji kutoka mtoni hadi mashambani kupitia bomba lililopo ambalo hutumia mashine ya diseli kuwahisha maji mashambani, mfumo anaosema ni ghali.
Kwa Munga Mazera , imewabidi kununua mabomba ya kufyonza maji chache yanayopatikana karibu na mitaro kuu ya maji, hilo akisema ni kwa wale wenye uwezo na walio karibu na mitaro kuu ya maji. Aidha ameeleza kusikitika na masaibu wanayopitia ikiwemo kukosa fidia ya mazao yanapokauka licha ya kutozwa ada za maji ilhali mradi wa serikali kuu wa Gravity upo umbali wa kilomita hamsini tu kuingia mashambani mwao. "Eneo la Nanighi Gravity inakoanza ni kilomita hamsini tu."Ameeleza kwa masikitiko.
Sasa wakulima hao wametaka serikali kuu kuharakisha mradi huo ili kuwanusuru na umasikini unaowakodolea macho licha ya kuchanika kwenye mpini. "Hii shida imechangikiwa na kutumia pump za diseli ambayo ni gharama, laiti Gravity ingekuwepo ingesuluhisha hii shida." Amesema Muchai.
"Hii Gravity tulianza kuisikia tangu nikiwa msichana, sasa nimekuwa mama nina watoto wanaonitegemea, tunahitaji kujifanyia kazi hatutaki kutegemea misaada." Ameongeza Grace.
Hata hivyo, kulingana na usimamizi wa mashamba ya NIA Bura maji husambazwa kwa wakulima kulingana na mfumo wa utaratibu waliokubaliana kati ya pande zote mbili, tofauti na awali walipokuwa wakipanda mahindi. Mamlaka hiyo imebaini kwamba maji hukatizwa jumamosi saa kumi na mbili jioni hadi jumapili saa kumi na mbili jioni ili maji yaelekezwe katika matumizi ya nyumbani mjini Bura na viunga vyake.
Mradi wa Gravity canal ulioanzishwa na serikali mwaka 2013 ulitarajiwa kuinua kilimo eneo la Bura kwa kupunguzia wakulima ada za kusambaziwa maji ambayo imekuwa ikifanywa kwa kutumia mashine za diseli ambayo inagharamu mafuta na utunzaji wake.
Mapema mwaka huu kamishena wa kaunti ya Tana River Thomas Sankei alikagua mradi huo ambao kwa wakati huo ulikuwa asilimia 60 na 27 kukamilika awamu ya kwanza na pili mtawalia,awamu ya tatu ya kulainisha mkondo uliopo mashauriano yake yakiwa mezani, kwa mujibu wa meneja wa mashamba ya NIA mjini Bura Peter Orwa.
Kwa mujibu wa Maur Bwanaka, mwaniaji wa kiti cha seneti Tana River ni jambo la kusikitisha wakulima kupitia masaibu waliyosimulia hivyo amependekeza kuundwa kwa kamati za maendeleo ya wakulima katika kaunti zitakazoangazia maslahi yao ikiwemo maswala ya kisheria huku akiwataka wakulima kunuia kuunda vyama vya ushirika kupiga jeki kilimo biashara.
Comments
Post a Comment